Wakati habari za shambulio la risasi dhidi ya Tundu Lissu zikihamia kwa viongozi wa kidini, Chadema imeeleza gharama zilizotumika hadi sasa kuokoa maisha yake na kuweka bayana kuwa imemuhamishia dereva wake nje ya mipaka kumuepusha na waliofanya shambulio hilo.
Lissu, mwanasiasa ambaye hana woga wa kuzungumza analoamini, alishambuliwa kwa risasi zipatazo 32 wakati akiwa kwenye gari lake lililoegeshwa nje ya majengo ya nyumba anayoishi akiwa Dodoma wakati wa shughuli za Bunge.
Risasi tano zilimpata mwilini, lakini akaepuka kifo na kwa sasa amelazwa Hospitali ya Aga Khan jijini Nairobi, ambako hali yake imeelezwa kuwa nzuri.
Taarifa ilkiyotolewa na mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe jana jioni pia imeeleza sababu za kumhamishia Lissu Hospitali ya Aga Khan ya jijini Nairobi, Kenya kutoka Hospitali ya Mkoa wa Dodoma na kushukuru wote waliohusika kuokoa maisha yake.
“Maisha ya Mhe Lissu yalikuwa hatarini sana na palihitajika matibabu maalumu na ya haraka sana kutoka kwa madaktari bingwa,” inasema taarifa hiyo.
Imeongeza kuwa matibabu yake pia yalihitaji vifaa tiba visivyo na shaka yeyote ili kuokoa maisha yake baada ya “kazi na kubwa na ya kupongezwa ya awali iliyofanywa na madaktari wetu kadhaa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma”.
Imeongeza kuwa jana, Lissu alikuwa akifanyiwa upasuaji mwingine.
“Hofu kuu ya usalama wa Mhe Lissu na dereva wake ilitanda kote nchini Tanzania baada ya shambulio dhidi ya uhai wao kushindwa kufanikiwa,” anasema Mbowe katika taarifa hiyo.
“Busara ya kiusalama ilitulazimisha kuwatoa wahanga nje ya mipaka ya nchi hadi hapo usalama wao utakapohakikishwa.
Mbowe anasema shambulio hilo lilimuumiza sana Lissu na ameokoka kimiujiza.
“Kutokana na ukweli huu, matibabu yake vilevile ni maalum na yanayohitaji wataalam wengi, vifaa tiba maalum na gharama kubwa,” anasema.
“Hadi sasa, zaidi ya Sh.100 milioni zimeshatumika kuokoa maisha ya ndugu yetu Lissu.
“Thamani ya Mhe. Lissu, ni kubwa kuliko kiwango chochote cha fedha. Kila njia iliyo halali itatumika kupata fedha za kutosha kumtibu Mhe. Lissu na hatimaye kumrudisha kwenye uwanja wa kudai haki, demokrasia na ustawi kwa wote nchini Tanzania.”
Taarifa hiyo inasema “dereva wa Mhe. Lissu, Simon Mohamed Bakari naye tunaye hapa Nairobi akiendelea kupata huduma za kisaikolojia”.
“Alishuhudia shambulio lile na aliokoka kimiujiza. Anasumbuliwa na msongo mkubwa wa mawazo. Naye hatukuona busara kuendelea kumuacha nchini hadi hapo hali yake ya kiafya na kiusalama itakapohakikishwa,” anasema Mbowe.
“Ni dhahiri kwa aina ya shambulio lilivyokuwa, wauaji walikusudia kuwaua wote; Mhe. Lissu na hata dereva wake.”
Chadema imerejea mazungumzo baina ya Serikali na chama hicho kuhusu hospitali gani apelekwe kutoka Dodoma.
“Upande wangu na Wabunge wetu wa Ukawa ulisisitiza Mhe. Lissu apelekwe moja kwa moja Nairobi na kama Bunge na Serikali hawatakuwa tayari kubeba gharama za kuokoa maisha ya Mhe. Lissu, basi sisi na Watanzania wenye mapenzi mema watachangia gharama hizo za kuokoa maisha kitibabu na kiusalama,” amesema Mbowe.
Mbowe amesema Lissu alitibiwa na madaktari wapatao kumi wa fani tofauti baada ya kufika Nairobi na walifanya kazi hiyo usiku kucha na anaendelea kutibiwa muda wote akiwa chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi wa karibu, lakini juzi aliweza kuzungumza.
“Kwa mara ya kwanza, Mhe. Lissu aliongea jana jioni na mkewe Alucia na baadaye na mimi, akisema ‘mwenyeki, I survived to tell the tale (niliokoka ili nisimulie mkasa). tafadhari, endeleeni kupambana”.
Amesema watu kutoka sehemu mbalimbali wamekuwa wakitaka kumtemebelea, lakini hawaruhusiwi na ulinzi umeimarishwa katika eneo analotibiwa.
“Hairuhusiwi wageni kumuona hadi hapo madaktari wakiridhika kuwa hali yake ya kimatibabu inaruhusu,” alisema.
Chadema imeeleza katika taarifa hiyo kuwa Tanzania si Salama, ikirejea mauaji ya mwenyekiti wa chama hicho mkoani Geita, Alphonce Mawazo aliyeuawa mwaka 2015, kamatakamata za wanaharakati na kuteswa kwa kilichoitwa makosa ya kimtandao.
Pia imetaja kutoweka kwa mshauri wa Mbowe, Ben Saanane na kutekwa kwa wasanii na kuteswa; kutaifishwa kwa mali, mashamba na biashara za viongozi wa upinzani.
Source: Mwananchi
Na:Esko Donald
Monday, 11 September 2017
MILLION 100 ZATUMIKA KUOKOA MAISHA YA LISSU.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
JIFUNZE KUPITIA HADITHI.
…JESCA…… Episode 4 Na:Esko Donald Esko Wa Simulizi 'EWS' Whatsapp:0675730796 Ilipoishia… Kwa muda huo watu wote walikuwa wapo ...

-
Linapojatwa jina la Director Nisher bila shaka itakuwa unakumbuka video ya nyimbo ya Young D "Kijukuu" na nyingine nyingi ambazo z...
-
Na:Esko Donald. Esko Wa Simulizi 'EWS'. Jesca binti wa Kimasai mwenye rangi ya bahati kuliko mabinti wote kijijini kwao alikuwa ni...
-
Madrid yafanikiwa kuandika historia mpya baada ya kulichukua kombe hili mara mbili mfululizo.
-
Bila shaka ni wengi hatumfahamu Lemma Guya Gemeda,huyu ni mchoraji maarafu kutoka nchini Ethiopia.Lemma ana umri wa miaka 90 na amechora zai...
-
……JESCA…… Episode ya 2 Na:Esko Donald. Esko Wa Simulizi 'EWS'. Whatsapp:0675730796. Ilipoishia.. BAADA YA MIAKA MITATU. Jesca...
No comments:
Post a Comment